Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limewakamata watu sita (6) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya aliyekuwa dereva bodaboda Hamisi Nchambi (27), ambaye mwili wake ulikutwa Januari 14, 2026 katika makaburi ya Miemba, Kata ya Mbugani, Manispaa ya Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Constantine Mbogambi, amesema watuhumiwa walikamatwa wakiwa na pikipiki ya marehemu aina ya SINORAY, rangi nyeusi, usajili MC 945 FHY, yenye thamani ya shilingi milioni 2.7. Inadaiwa walimkodi kama abiria, kisha kumpeleka makaburini na kumuua kwa kumnyonga.
Katika tukio jingine, polisi wamewakamata watu wanne (4) waliokutwa na vifaa vya wizi vilivyoibwa katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria, huku watuhumiwa wengine watano (5) wakikamatwa awali wakiwa na pikipiki tisa (9) zilizoibwa maeneo ya Tabora na Shinyanga.
Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na operesheni za kukabiliana na uhalifu na kutoa wito kwa wananchi kujihusisha na shughuli halali.
Chanzo; Global Publishers