Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Serikali Yapunguza Ada Leseni ya Watoa Maudhui Mtandaoni

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepunguza ada za leseni kwa watoa huduma na wakusanya maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikikabili sekta hiyo na kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidigitali.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji 2026 unaofanyika Dodoma kwa siku mbili kuanzia Februari 12, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema Serikali iliagiza TCRA kufanya mapitio ya ada hizo kufuatia malalamiko ya wadau kuhusu gharama kuwa kubwa.

Amesema mapitio hayo yamekamilika na kuleta nafuu kwa watoa maudhui, hususan vijana wabunifu na wajasiriamali wa majukwaa ya mtandaoni.

“Nafuraha kuwafahamisha kwamba ada za leseni kwa watoa maudhui mtandaoni zimepunguzwa kutoka Sh 500,000 hadi Sh 50,000, na ada ya maombi ni Sh 10,000 tu. Kwa wakusanya maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepungua kutoka Sh milioni moja hadi Sh 100,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh 20,000,” amesema Mwinjuma.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhamasisha urasimishaji wa shughuli za kidigitali, kupanua fursa kwa vijana, kuchochea ajira na kuongeza mchango wa uchumi wa kidigitali katika pato la taifa.

Katika hatua nyingine, Mwinjuma amesisitiza kuwa mafunzo kwa waandishi wa habari hayawezi kuleta matokeo chanya iwapo maslahi yao hayatazingatiwa. Amebainisha kuwa baadhi yao hawana mikataba rasmi na hulipwa stahiki zao kwa kuchelewa.

“Naiagiza TCRA kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unaenda sambamba na uthibitisho wa mikataba na malipo stahiki kwa wafanyakazi,” amesema.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kushughulikia madeni ya matangazo ya Serikali yanayodaiwa na vyombo vya habari ili yalipwe kwa wakati na kusaidia mzunguko wa fedha katika sekta hiyo.

 

 

Chanzo; Nipashe

Kuhusiana na mada hii: