Watu 31 wamefariki dunia nchini Lebanon kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel ambayo yamelenga maeneo ya makazi katika mji mkuu Beirut na kusini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Machi 2, 2026 na Wizara ya Afya imeeleza kuwa watu 149 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyolenga ngome za Hezbollah, kundi la wanamgambo wa Kishia nchini humo.
Mashambulizi hayo yanakuja baada ya Hezbollah kurusha makombora kuelekea mji wa bandari wa Haifa nchini Israel usiku wa jana, tukio lililosababisha jeshi la Israel kujibu kwa operesheni ya anga.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), Eyal Zamir, amesema operesheni hiyo imeanza rasmi na inaweza kudumu kwa siku kadhaa.
“Tumeyaanza mashambulizi dhidi ya Hezbollah… tunajiandaa kwa siku kadhaa za mapigano,” amesema.
Kwa mujibu wa jeshi la Israel, maeneo yaliyolengwa ni pamoja na vitongoji vya kusini mwa Beirut vinavyotajwa kuwa ngome kuu ya Hezbollah pamoja na maeneo ya karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji huo.
Chanzo; Mwananchi