Mahakama Kuu ya Zambia imeamuru kukamatwa kwa mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 1.3 sawa na (Sh. Bilioni 3.3) kutoka kwa Dalitso Lungu, ambae ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa zamani wa taifa hilo Edgar Lungu.
Agizo la ukamataji wa mali hizo linajumuisha magari 79 na vipande 23 vya ardhi na mali isiyohamishika, ikiwa ni pamoja na maduka makubwa, kituo cha mafuta, ghorofa za kifahari na makao makuu katika mji mkuu wa Lusaka.
Hukumu hiyo ilisema mtu huyo mwenye umri wa miaka 39 na kampuni yake wameshindwa kutoa maelezo ya kuaminika na yanayoweza kuthibitishwa kuhusu jinsi mali hizo zilivyopatikana kihalali.
Edgar Lungu, ambaye aliongoza Zambia kwa miaka sita kutoka 2015, alifariki nchini Afrika Kusini Juni mwaka jana lakini bado hajazikwa kwa sababu ya vita vya kisheria vinavyoendelea kati ya familia yake na serikali ya sasa.
Chanzo; Nipashe