Shirika la usalama wa baharini la Uingereza limeonya kwamba washambuliaji walipanda meli karibu na pwani ya Somalia siku ya Alhamisi, baada ya matukio mawili ya hivi karibuni kuzua hofu ya kuibuka tena kwa uharamia.
Meli hiyo, inayoendeshwa na kampuni ya Ugiriki ya Latsco Marine Management, ilishambuliwa muda mfupi kabla ya adhuhuri na washambuliaji wenye silaha ilipokuwa ikisafiri kwenda Afrika Kusini kutoka India.
Kampuni hiyo ilisema katika taarifa kwamba wafanyakazi wote 24 wako salama na wanahesabiwa, na wanaendelea kuwasiliana nao kwa karibu, huku ikikataa kutoa taarifa zaidi kwa sababu za kiusalama.
Kituo cha Operesheni za Biashara za Baharini cha Uingereza (UKMTO) kilisema mashua hiyo, Hellas Aphrodite, ilikaribiwa kutoka nyuma na meli ndogo, kabla ya kuingiliwa na wafanyakazi ambao hawakuwa na idhini. Mamlaka wanachunguza kisa hicho. Kikosi cha wanamaji cha Umoja wa Ulaya kinachopambana na uharamia kimesema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X kwamba kilikuwa karibu na tukio hilo na kiko tayari kuchukua hatua zinazofaa ili kujibu ipasavyo tahadhari hii ya uharamia.
Chanzo; Dw