Akiongelea kuhusu hatma ya utawala wa Venezuela, Rais Donald Trump alisisitiza kuwa Marekani itaiongoza Venezuela mpaka pale watakapoona kuna usalama wa kutosha kuiachia nchi kwa utawala mpya.
Trump alisema hayo masaa machache baada ya jeshi lake kumkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mke kwa madai mbalimbali ikiwemo kuhusika na biashara ya madawa ya kulevya na kuminya uhuru wa wananchi.
“Hatutaki kuona mtu mwingine anashika madaraka, na kuanza kutupa tabu kama tuliyoipata kwa miaka mingi iliyopita. Kwahiyo tunaenda kuongoza nchi hiyo, tutaendesha nchi hadi wakati ambapo tunaweza kufanya mabadiliko salama, sahihi na ya busara, na lazima yawe ya busara, “aliongeza Trump.
Alipoulizwa swali kwamba itakuwaje endapo Marekani itajikuta inaiongoza Venezuela kwa miaka mingi, Trump alijibu kuwa “haitatugharimu chochote kwa sababu pesa inayotoka ardhini (mafuta) ni nyingi.”
Hata hivyo, Trump aliongeza kuwa Marekani iko tayari kufanya mashambulizi mengine makubwa zaidi Venezuela pale itakapobidi, na tayari makampuni makubwa ya mafuta ya Kimarekani yamejipanga kwenda Venezuela na kutumia mabilioni ya dola kujenga upya miundombinu ya mafuta iliyoharibika.
Kuhusu jeshi la Venezuela, Trump alisema kwamba uwezo wote wa kijeshi wa Venezuela haukuwa na nguvu kwani wanaume na wanawake wa jeshi la Marekani walifanikiwa kumkamata Maduro usiku wa manane bila shida yoyote.
Chanzo; Clous Media