Serikali ya Kenya imekemea vikali vitendo vya mawakala wanaodanganya vijana kwa ahadi za kazi nchini Urusi, kisha kuwapeleka moja kwa moja kwenye vita vinavyoendelea Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema anatarajia kufanya ziara rasmi mjini Moscow kwa mazungumzo na Serikali ya Urusi, akilenga kusitisha kabisa matumizi ya raia wa Kenya katika mapambano hayo.
Mudavadi amesema tayari Wakenya kadhaa wamefariki dunia huku wengine wakijeruhiwa vibaya baada ya kudanganywa kuingia mikataba ya kijeshi. Aidha, Kenya imewalaumu mawakala wa ajira wanaowashawishi vijana kwa ahadi za mishahara mikubwa, kisha kuwapeleka mstari wa mbele vitani.
Ripoti ya hivi karibuni ya shirika la habari la Ufaransa, Agence France-Presse, imebaini mtandao wa udanganyifu uliowanasa vijana wasiokuwa na historia ya kijeshi, wakilazimishwa kusaini mikataba na jeshi la Urusi kabla ya kupelekwa haraka uwanja wa mapambano Ukraine.
Mudavadi amesema Kenya itafuatilia pia suala la kuachiliwa kwa Wakenya waliokamatwa kama wafungwa wa kivita nchini Ukraine, akisisitiza kuwa upotevu wa maisha haukubaliki na lazima hatua za kudumu zichukuliwe.
Chanzo; Global Publishers