Maelfu wananchi wa Mexico wameandamana jumamosi hii Novemba 15 mpaka nje ya Ikulu ya Mexico anakoishi Rais wa nchi hiyo Claudia Sheinbaum, wakipinga uhalifu, rushwa na kutokujali kwa serikali yake.
Maandamano hayo yaliandaliwa na vikundi vya vijana vya Gen Z, wakipata uungwaji mkono kutoka kwa raia wanaopinga mauaji ya watu mashuhuri, ikiwa ni pamoja na mauaji ya wiki chache zilizopita ya Meya wa Uruapan, Carlos Manzo, ambaye alikuwa ametaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya magenge ya uhalifu.
Maandamano hayo mengi yalikuwa ya amani lakini yalimalizika kwa baadhi ya vijana kupigana na polisi. Waandamanaji waliwashambulia polisi kwa mawe, fataki, fimbo na minyororo, kunyakua ngao za polisi na vifaa vingine.
Katibu wa usalama wa mji mkuu, Pablo Vázquez alisema watu takribani 120 walijeruhiwa, 100 kati yao ni maafisa wa polisi. Pia watu 20 walikamatwa. Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum alisema maandamano hayo yaliyofanyika pia katika miji mingine, yamefadhiliwa na wanasiasa wa upinzani wanaopinga serikali yake.
Chanzo; Tanzania Journal