Tangazo la Marekani kujiondoa rasmi uanachama katika Shirika la Afya Duniani (WHO), limeongeza wasiwasi duniani katika kukabiliana na majanga ya kiafya.
Uamuzi wa Marekani, ambayo ilikuwa inachangia fedha nyingi za ufadhili, umeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa WHO na utendaji kazi wake katika kudhibiti na kulinda afya za watu duniani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, mwaka jana alitia saini agizo la kujiondoa katika shirika hilo, akidai kuipendelea China wakati wa mlipuko wa Covid-19.
Hatua ya kujiondoa uanachama ilianza kutekelezwa jana na kusitisha mchango wa kifedha na ushirikiano wa moja kwa moja kati ya Marekani na WHO.
Taarifa ya Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Marekani, ilisema uamuzi huo ulitokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushindwa kwa WHO kushughulikia ipasavyo janga la Covid-19 na kukosa kufanya mageuzi ya ndani.
Sababu nyingine ni taasisi hiyo kuathiriwa na shinikizo la kisiasa kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama. Ilisema taarifa hiyo kuwa serikali ilisitisha kabisa ufadhili wake kwa WHO kwa kuwarejesha wafanyakazi na wakandarasi wake kutoka makao makuu ya WHO yaliyoko mjini Geneva, nchini Uswizi.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa serikali ya Marekani imesimamisha mawasiliano yote rasmi kati ya pande hizo mbili. Walisisitiza kuwa kujiondoa huko ni hatua ya kulinda maslahi ya taifa lao.
Katika taarifa ya pamoja, Waziri wa Afya wa Marekani Robert F. Kennedy na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, walisema kuwa WHO ilipuuza na kufuta kila kitu ambacho Marekani imeifanyia.
Chanzo; Nipashe