Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Ajaribu Kumbusu Rais Atiwa Mbaroni

Mwanaume mmoja, anayejulikana kwa jina la Uriel Rivera Martínez, amekamatwa na vyombo vya usalama nchini Mexico baada ya kumvamia Rais Claudia Sheinbaum katika hafla ya umma karibu na Ikulu ya Taifa jijini Mexico City. Tukio hilo lilitokea mbele ya umati wa watu na lilinaswa kwenye video inayoonyesha mwanaume huyo akijaribu kumbusu rais kwa nguvu, kitendo kilichomfanya Sheinbaum amsukume kwa haraka kabla ya walinzi wake kuingilia kati na kumdhibiti mshambuliaji huyo.

Kisa hicho kimezua hisia kali nchini humo, hasa kutokana na namna kilivyomhusisha kiongozi mkuu wa taifa. Mshukiwa huyo kwa sasa anashikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia na ukiukaji wa usalama wa rais.

Baada ya tukio hilo, Rais Sheinbaum amewasilisha malalamiko rasmi dhidi ya mshambuliaji wake na kutoa kauli yenye uzito akisisitiza kuwa aliamua kuchukua hatua “kama mwanamke na kwa niaba ya wanawake wote wa Mexico.” Aidha, alitoa wito kwa wabunge na taasisi za sheria kuharakisha mchakato wa kuweka adhabu kali kwa makosa ya unyanyasaji wa kijinsia, ili kuwalinda wanawake wote dhidi ya vitendo kama hivyo vinavyoendelea kukithiri nchini humo.

Tukio hilo limeibua upya mjadala mkali kuhusu ukosefu wa usalama wa wanawake na utamaduni wa machismo unaotawala katika jamii ya Mexico. Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa takribani asilimia 70 ya wanawake nchini humo wamewahi kupitia aina fulani ya udhalilishaji au unyanyasaji wa kijinsia, jambo linaloendelea kuwa changamoto kubwa kijamii na kisiasa.

Wachambuzi wa masuala ya usalama na haki za wanawake wamesema kuwa tukio hilo linapaswa kuwa kengele ya tahadhari kwa serikali, hasa kwa kuzingatia udhaifu ulioonekana katika ulinzi wa rais. Wameitaka serikali kuimarisha mikakati ya usalama kwa viongozi na raia kwa ujumla, sambamba na kuendeleza kampeni za kubadilisha mitazamo ya kijinsia inayowadhalilisha wanawake.

 

Chanzo; Global Publishers

Kuhusiana na mada hii: