Shirika la Anga la Marekani NASA linaendelea na mipango ya kurudisha wanadamu kwenye Mwezi kwa mara ya kwanza tangu enzi za Apollo.
Taarifa mpya zinaonyesha kuwa shirika hilo linaelekea kupiga hatua muhimu baada ya kutangaza mpango wa kuzindua misheni ya Artemis II mapema mwezi Machi.
Hii ni hatua inayosubiriwa kwa shauku kubwa duniani kote, ikizingatiwa kuwa safari ya mwisho ya binadamu kuuzunguka Mwezi ilifanyika zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Mara ya mwisho wanadamu kusafiri karibu na Mwezi ilikuwa mwaka 1972, kupitia misheni ya Apollo 17. Tangu wakati huo, safari za binadamu zimekuwa zikibaki katika mzingiro wa dunia pekee.
NASA imeweka tarehe ya mapema zaidi ya uzinduzi kuwa Machi 6. Tarehe hiyo imewekwa baada ya mafanikio ya jaribio muhimu linalojulikana kama "wet dress rehearsal."
Artemis II ni misheni ya pili katika mpango mpana wa Artemis, unaolenga kumrudisha binadamu kwenye uso wa Mwezi na hatimaye kuweka msingi wa safari za baadaye kuelekea Mars.
Chanzo; Dw