Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Burkina Faso, Mali, Niger Wajiondoa ICC

Burkina Faso, Mali na Niger yametangaza kujiondoa mara moja kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), yakiituhumu taasisi hiyo kwa kuendeleza ukoloni mambo leo na ubaguzi katika utekelezaji wa haki. Mataifa haya matatu ya ukanda wa Sahel yameeleza kuwa ICC imekuwa chombo cha kuwaandama viongozi wa mataifa masikini, hasa barani Afrika, huku ikishindwa kuwachukulia hatua wahalifu wakuu duniani.

Katika taarifa ya pamoja iliyosainiwa na Jenerali Assimi Goïta, Rais wa Mali, mataifa hayo yamesema kuwa ICC imepoteza uhalali wake na imeshindwa kutimiza wajibu wake wa msingi wa kuhakikisha haki ya kweli kwa wote. Wamesisitiza kuwa mashambulizi ya mahakama hiyo yamewalenga viongozi wa Afrika, hali inayoonesha wazi kile walichokiita ubaguzi wa kimfumo.

Uamuzi huu ni mwendelezo wa hatua kali zinazochukuliwa na serikali za kijeshi zinazoongoza mataifa haya, ambazo tayari mwaka huu zilijiondoa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), na kuanzisha Jumuiya ya Mataifa ya Sahel (AES). Hatua hiyo mpya inaashiria msimamo wa pamoja wa kupinga kile wanachokiona kama ushawishi na udhibiti wa taasisi za kimataifa dhidi ya uhuru wa nchi zao.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyoundwa mwaka 2002, imepewa jukumu la kushughulikia kesi za mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Hadi sasa, mahakama hiyo imepokea jumla ya mashitaka 33, mengi yakiwa yanawahusu viongozi kutoka bara la Afrika.

Wakosoaji wa ICC wamekuwa wakilalamikia upendeleo, wakisema kuwa mahakama hiyo inawalenga zaidi viongozi wa Afrika huku ikikwepa kuwachunguza wale kutoka mataifa makubwa yenye ushawishi wa kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo, watetezi wa ICC wanasisitiza kuwa kutokana na udhaifu wa mifumo ya haki katika baadhi ya mataifa ya Afrika, mahakama hiyo inatoa fursa kwa waathiriwa wa uhalifu mkubwa kutafuta haki nje ya mipaka ya nchi zao.

 

Chanzo: Global Publishers

Kuhusiana na mada hii: