Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameapa kutokubali shinikizo baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuwasaidia waandamanaji. Matamshi yake yanatolewa wakati makundi ya haki za binadamu yakiripoti ongezeko kubwa la kukamatwa kwa watu kufuatia siku kadhaa za machafuko yaliyochochewa na kupanda kwa mfumuko wa bei.
Akizungumza kupitia hotuba iliyorekodiwa na kurushwa kwa njia ya Televisheni siku ya Jumamosi, Khamenei alisema Jamhuri ya Kiislamu haitasalimu amri dhidi ya adui yake na akasisitiza kuwa waandamanaji wanafanya fujo na wanapaswa kushughulikiwa.
Makundi ya haki za binadamu yanasema zaidi ya watu 10 wameuawa na kadhaa kukamatwa katika maandamano yaliyoenea kote Iran tangu siku Jumapili, huku sarafu ya rial ikizidi kuporomoka na kuathiri uchumi ambao tayari umedhoofishwa na vikwazo.
Chanzo; Nipashe