Njama ya kumuua kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, imezuiwa, limetangaza taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mpango huo ulikuwa umepangwa na Luteni Kanali Paul Henri Damiba, afisa wa kijeshi aliyeondolewa madarakani na Traoré Septemba 2022, amesema waziri wa usalama katika taarifa ya usiku wa manane.
"Shirika letu la kijasusi limezuia operesheni hii katika saa za mwisho. Walikuwa wamepanga kumuua mkuu wa nchi na kisha kushambulia taasisi zingine muhimu, wakiwemo watu mashuhuri," amesema Mahamadou Sana, akidai njama hiyo imeandaliwa nchi jirani ya Ivory Coast.
Hakuna taarifa yoyote kutoka kwa Kanali Damiba au Ivory Coast.
Tangu alipochukua madaraka, Kapteni Traoré amekabiliwa na majaribio mawili ya mapinduzi na pia anakabiliwa na ongezeko la vurugu za wanajihadi ambazo zimewalazimisha mamilioni ya watu kukimbia makwao.
Licha ya changamoto hizi, kiongozi huyo wa kijeshi mwenye umri wa miaka 37 ana uungwaji mkono mkubwa na amepata wafuasi kote Afrika kwa maono yake ya umajumui wa Kiafrika na ukosoaji wake wa nchi za Magharibi.
Kulingana na waziri wa usalama, serikali iligundua video iliyovuja ikiwaonyesha wapangaji wakijadili mipango yao.
Katika picha hizo, inadaiwa walizungumzia jinsi walivyokusudia kumuua rais - iwe karibu au kwa kuweka vilipuzi nyumbani kwake – siku ya Jumamosi tarehe 3 Januari.
Baadaye inadaiwa walipanga kuwalenga maafisa wengine wakuu wa kijeshi na raia.
Sana amedai Damiba amekusanya wanajeshi na wafuasi wa kiraia, akapata ufadhili wa kigeni - zaidi ya faranga milioni 70 za CFA ($125,000; £92,000) zilizotolewa kutoka Ivory Coast - na alipanga kuangamiza kambi ya ndege zisizo na rubani nchini humo kabla ya vikosi vya kigeni kuingilia kati.
"Tunafanya uchunguzi na tumewakamata watu kadhaa. Watu hawa watafikishwa mahakamani hivi karibuni," waziri huyo amesema kwenye televisheni ya taifa.
Haijulikani ni watu wangapi wamekamatwa.
Kanali Damiba alihudumu kama kiongozi wa Burkina Faso kuanzia Januari-Septemba 2022 baada ya kunyakua madaraka kutoka kwa serikali iliyochaguliwa kiraia.
Baada ya kufukuzwa alikwenda uhamishoni katika nchi jirani ya Togo na akasema katika ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba anamtakia mrithi wake kila la heri.