Mamlaka katika nchi 14 za Afrika zimewakamata watu 260 katika operesheni dhidi ya uhalifu wa kimtandao unaolenga udanganyifu wa kimapenzi na kulazimisha watu kujivua nguo mtandaoni.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Polisi wa Interpol, Cyril Gout amesema kuongezeka kwa uhalifu unachochewa na teknolojia barani Afrika.
Amesema operesheni hiyo imeonesha jinsi uhalifu wa kimtandao unavyokuwa tishio linalokua kwa kasi zaidi katika sekta ya usalama barani Afrika, na umuhimu wa hatua za pamoja ili kulinda usalama wa watu mtandaoni.
Operesheni hiyo ya wiki mbili, iliyoandaliwa na Interpool imefanywa kati ya Julai 28 na Agosti 11, 2025. Polisi wamekamata zaidi ya vifaa 1,200 vya kielektroniki, kufunga miundombinu 81 ya uhalifu mtandaoni na kubaini karibu waathirika 1,500 Afrika.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kutafuta wapenzi na kuwatapeli. Matukio ya udanganyifu wa kimapenzi yalihusisha wasifu bandia na picha zilizoibiwa, huku matukio kuonyesha utupu yakihusisha vitisho dhidi ya waathiriwa kwa kutumia video au picha zisizofaa walizotumiwa.
Ghana imeongoza kwa idadi ya waliokamatwa, ambapo watuhumiwa 68 walitiwa mbaroni na Dola 70,000 zilizokuwa zimeibwa zimerejeshwa.Nchini Senegal, watuhumiwa 22 wanadaiwa kujifanya watu mashuhuri ili kuwaibia waathiriwa 120. Polisi nchini Côte d’Ivoire walivunja mtandao wa sextortion uliokuwa umewaathiri watu zaidi ya 800.
Chanzo: Mwananchi