Dereva mmoja wa basi la London aliyemfukuza mwizi na kumpiga ngumi hadi akapoteza fahamu amefutwa kazi.
Mark Hehir, ambaye alikiambia kikao cha mahakama kwamba alizingatiwa kama "shujaa" na umma, alikuwa akiendesha basi wakati mwanaume mmoja alipoiba mkufu wa abiria.
Hehir alimfuata na kuuchukua mkufu huo, lakini akasema mwanaume huyo alirudi kwenye basi kumkabili, na akarusha "ngumi ya kwanza". Mahakama iliambiwa Hehir alirusha ngumi ili kujilinda kisha akamzuia mwanamume huyo kwa karibu "nusu saa". Mwanaume huyo alikuwa amerudi kwenye basi kuomba radhi. Wanaume hao wote walikamatwa, hata hivyo Hehir aliachiliwa huru baadaye.
Siku moja baada ya tukio hilo la tarehe 25 Juni 2024, Hehir alisimamishwa kazi na kuambiwa afike mahakamani.
Katika kikao cha kinidhamu, aliambiwa kuwa "aliichafua kampuni ya mabasi kwa kumshambulia abiria" na kwamba pia "alishindwa kulinda usalama wake na wa abiria wake kwa kuacha basi bila uangalizi huku injini ikiendelea kunguruma na kumfukuza mwizi".
Chanzo; Dw