Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameionya Marekani kuwa Tehran iko tayari kwa vita endapo Washington itaamua kuijaribu, akisisitiza kuwa nchi yake imejiandaa kwa hatua yoyote ya kijeshi kufuatia vitisho vya Rais Donald Trump vya kuchukua hatua dhidi ya ukandamizaji wa maandamano ya kupinga Serikali nchini Iran.
Akizungumza jana Januari 12, 2026 katika mahojiano maalumu na kituo cha Al Jazeera, Araghchi amesema licha ya machafuko yanayoendelea, njia za mawasiliano kati ya Iran na Marekani bado ziko wazi. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Iran ina uwezo mkubwa wa kijeshi na haitasita kujilinda endapo italazimika.
Kauli hizo zinajiri baada ya Trump kusema anafikiria kufanya maamuzi magumu dhidi ya Iran kutokana na hatua za viongozi wa nchi hiyo kukandamiza maandamano yanayoendelea.
Trump pia amesema kuna mpango wa kufanya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, lakini akaonya kuwa Marekani huenda ikachukua hatua kabla ya mazungumzo hayo kufanyika.
Araghchi amesema Iran iko tayari endapo Marekani itajaribu tena hatua za kijeshi ilizowahi kuzijaribu hapo awali, akieleza matumaini yake kuwa Washington itachagua njia ya busara ya mazungumzo.
Chanzo; Mwananchi