Mishumaa Yasababisho vifo Watu 40 Uswiss Waendesha mashtaka nchini Uswisi wanasema mishumaa maalum iliyotumika kusheherekea mwaka mpya huenda ndiyo kichoosababisha moto ulioua zaidi ya watu 40 katika baa ya Le Constellation, Uswisi wakati wa sherehe za kuukaribisha Mwaka Mpya.
Mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la Valais, Beatrice Pilloud (pichani), alisema ushahidi wa awali unaonyesha mishumaa hiyo aina ya fountain candles ilikuwa imefungwa kwenye chupa za shampeni na ilikuwa imewekwa karibu sana na dari ya baa hiyo.
Alisema moto ulianza kwa haraka na kusambaa kwa kasi kubwa, hali iliyozidishwa na mazingira ya ndani ya jengo, na kusababisha waliokuwemo kukosa muda wa kutosha kujiokoa.
Wachunguzi wanaendelea kukagua mabaki ya baa hiyo, kuchambua video zilizorekodiwa na kusambazwa mitandaoni, pamoja na kuwahoji manusura ili kubaini kwa uhakika chanzo cha moto huo.
Uchunguzi huo pia unaangazia ukarabati uliowahi kufanyika katika jengo hilo, aina ya vifaa vilivyotumika hususani vifaa vya kuzuia kelele vilivyowekwa kwenye dari, pamoja na mifumo ya kukabiliana na moto na njia za kutokea wakati wa dharura.
Wamiliki wa baa hiyo wamesema marekebisho yote yalifanywa kwa kuzingatia kanuni za usalama, huku waendesha mashtaka wakisisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea na hakuna hitimisho la mwisho lililotolewa.
Chanzo; Global Publishers