Kijana wa miaka 22 kutoka Utah amekamatwa kwa mauaji ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia Charlie Kirk, ambaye alipigwa risasi akiwa jukwaani kwenye hafla ya chuo kikuu mapema wiki hii.
Tyler Robinson aliwekwa kizuizini siku ya Alhamisi usiku, baada ya msako wa saa 33 ambao ulikamilika babake aliposaidia kumshawishi ajisalimishe kwa polisi.
Kukamatwa kwake kulitangazwa kwa mara ya kwanza na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alimtaka mshukiwa huyo kukabiliwa na hukumu ya kifo.
Mauaji ya Kirk, ambaye alipigwa risasi alipokuwa akijadiliana na wanafunzi siku ya Jumatano, yamewashtua Wamarekani na kuweka wazi migawanyiko mikali juu ya vyama nchini humo.
Wachunguzi walisema katika kikao na wanahabari siku ya Ijumaa kwamba mshukiwa alikiri kwa baba yake na kusema afadhali ajiue badala ya kujisalimisha. Kisha baba huyo alimwita mchungaji kijana ambaye ni rafiki wa familia.
Wote wawili walijaribu kumtuliza mshukiwa, polisi walisema. Mchungaji huyo, ambaye pia anahudumu kama afisa wa usalama wa mahakama, baadaye aliwapigia simu wanajeshi wa Marekani, ambao walimshika mshukiwa mwendo wa saa 22:00 kwa saa za eneo siku ya Alhamisi.
Gavana wa Utah Spencer Cox alisema kuwa picha za uchunguzi zilionyesha Bw Robinson akiwasili katika chuo kikuu cha Utah Valley takriban saa nne kabla ya tukio la mlio wa risasi kushuhudiwa, na kumuua Kirk huku wanafunzi kukikimbia kujificha.
Cox aliwaambia waandishi wa habari kwamba wakati Bw Robinson aliwekwa kizuizini, alikuwa amevalia mavazi sawa na yale yaliyoonekana kwenye kamera za CCTV katika eneo la ufyatuaji risasi.
Gavana huyo aliongeza kuwa wachunguzi walimhoji mwanafamilia, ambaye alisema mshukiwa huyo amekuwa wa siasa kali katika miaka ya hivi majuzi.
Cox alisema mwanafamilia huyo alizungumza kuhusu tukio la hivi majuzi wakati Bw Robinson alipotaja kwamba Kirk alikuwa anakuja Utah na kwamba "alikuwa amejaa chuki na kueneza chuki".
Cox alisema wachunguzi pia walikuwa wamezungumza na mshukiwa aliyeishi naye chumba kimoja ambaye aliwaonyesha ujumbe waliobadilishana naye kwenye akaunti inayoitwa "Tyler" kwenye programu ya ujumbe ya Discord.
Jumbe hizo zilirejelea hitaji la kupata bunduki kutoka "sehemu moja" na bunduki hiyo kuachwa kwenye kichaka, ikiwa imefungwa kwa taulo.
FBI walisema siku ya Alhamisi kwamba walipata silaha inayoshukiwa kuwa - bunduki aina ya Mauser .30-06 bolt action - ikiwa imefungwa kwa taulo katika eneo lenye miti karibu na chuo kikuu.
Chanzo: Bbc Swahili