Mbunge wa kujitegemea Dan Norris (66), nchini Uingereza amekamatwa kwa mara ya pili akituhumiwa kwa makosa ya kingono ikiwemo kumbaka mwanamke na kuwachungulia wanawake kadhaa.
Imeelezwa kuwa mbunge huyo ambae pia alikuwa Meya wa zamani wa Magharibi mwa Uingereza anachunguzwa na vyombo vya usalama kwa kufanya unyanyasaji wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika mbunge huyo alikamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 2025 kwa tuhuma za makosa ya kingono dhidi ya msichana, utekaji nyara wa mtoto, na ubakaji wa mwanamke. Makosa yote yanadaiwa kutokea kati ya miaka ya 2000 na 2020.
Norris pia anachunguzwa kwa utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma, na kwamba kwa sasa yuko nje kwa dhamana.
Alichaguliwa kuwa mbunge wa chama cha Labour katika jimbo la North East Somerset na Hanham mwezi Julai 2024, akimshinda mbunge wa chama cha Conservative Jacob Rees-Mogg.
Chama cha Labour kilimsimamisha kazi Norris mara moja kilipofahamishwa kuhusu kukamatwa kwake mwezi Aprili.
Licha ya kusimamishwa kwake, Norris amekataa kujiuzulu kutoka nafasi yake kama mbunge, na kwamba ombi linalomtaka ajiuzulu limepata zaidi ya sahihi 2,000.
Norris kwa sasa ni mbunge huru lakini hajahudhuria Bunge la Commons tangu alipokamatwa. Ikielezwa kuwa atapoteza nafasi yake kama mbunge ikiwa atashtakiwa, kuhukumiwa na kufungwa jela.
Norris pia alikuwa meya wa Magharibi mwa Uingereza alipokamatwa kwa mara ya kwanza. Muhula wake uliisha Mei 2025. Polisi walisema uchunguzi wao kuhusu Norris ulianza Desemba 2024.
Chanzo; Nipashe