Wakati maandamano yakiendelea nchini Iran Kiongozi wa taifa hilo, Ali Khamenei amesema waandamanaji katika taifa hilo wanaandamana ili kumfurahisha Rais wa Marekani, Donald Trump.
Akizungumza na wafuasi wake mapema asubuhi ya leo, Khamenei aliwapuuza waandamanaji na kuwaita "kundi la waharibifu" wanaotaka "kumfurahisha" Rais wa Marekani Donald Trump.
Katika hotuba ya video iliyotangazwa kwenye televisheni ya kitaifa, Khamenei alisema:
"Kundi la waharibifu lilijitokeza Tehran na maeneo mengine na kuharibu majengo ya nchi yao ili kumfurahisha rais wa Marekani."
"Hiyo ni kwa sababu alitoa madai ya kipuuzi kwamba anawaunga mkono ninyi waandamanaji na watu ambao ni hatari kwa nchi. Kama ana uwezo, anapaswa kuendesha nchi yake mwenyewe." amesema Khamenei
Trump amekuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa Iran kwa muda mrefu na aliahidi kuingilia kati ikiwa raia watauawa katika maandamano hayo.
Chanzo; Nipashe