Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara amemteua mdogo wake, Tene Ouattara kushika wadhifa mpya ulioundwa wa naibu waziri mkuu.
Hatua hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti nchini humo, ikitafsiriwa kama sehemu ya mabadiliko makubwa ya kisiasa ndani ya serikali yake.
Uteuzi huo uliofanyika Ijumaa ya Januari 23, 2026 ni mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyopewa jina la Mambe II, yaliyofanyika siku mbili tu baada ya Robert Mambe kuthibitishwa tena kuwa waziri mkuu kufuatia ushindi wa chama tawala katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika Desemba 2025.
Tene Ouattara anayejulikana kwa jina la utani Photocopy kutokana na kufanana kwake kwa karibu na Rais atahudumu katika wadhifa huo mpya wa juu, huku akiendelea kubaki pia kama waziri wa ulinzi nafasi yenye ushawishi mkubwa ndani ya serikali na vyombo vya usalama vya taifa.
Chanzo; Mwananchi