Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy ameachiwa gerezani, ikiwa ni wiki tatu tu katika kifungo chake cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki katika njama ya uhalifu. Atakuwa chini ya uangalizi wa mahakama huku akiwa haruhusiwi kuondoka Ufaransa kabla kesi yake ya rufaa itakaposikilizwa mwaka ujao.
Oktoba 21, 2025, rais huyo mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kuhusika katika njama ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa 2007 kwa fedha zilizotolewa na rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi.
Baadaye, timu yake ya wanasheria iliwasilisha ombi la rufaa ili aachiliwe. Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachiliwa, Sarkozy amesema: "Nguvu zangu ziko katika lengo moja la kuthibitisha kutokuwa na hatia. Ukweli utashinda… Mwisho wa hadithi bado haujaandikwa."
Gari la Sarkozy limeonekana likitoka kwenye Gereza la La Santé, mjini Paris, chini ya saa moja na nusu baada ya mahakama kukubali kuachiliwa kwake. Muda mfupi baadaye, alionekana akiwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris.
Chanzo; Mwananchi