Ofisi ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema imepinga hatua ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini Burkina Faso, uamuzi uliofanywa na utawala wa kijeshi unaoongoza taifa hilo kwa sasa.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ametaka nafasi halisi ya kiraia na kidemokrasia iheshimiwe nchini humo, kauli inayokuja baada ya Januari 29 utawala wa kijeshi Burkina Baso kutangaza hatua ya kuvunja vyama hivyo
“Hii si hatua katika mwelekeo sahihi kwa haki za binadamu kwa raia wa Burkina Faso,” alisema Turk, ambaye wakati wa ziara yake ya mwisho mwezi Juni 2024 alitoa wito wa uchunguzi kuhusu mauaji ya raia na kwamba haujawahi kufanyika.
Anadai kwamba utawala wa kijeshi ambao hauheshimu tena maamuzi ya mahakama, unakandamiza uhuru wa vyama vya wafanyakazi, na unawakamata kikatili wapinzani na wakosoaji.
“Badala ya kupiga marufuku vyama vya siasa na kuwafunga watu, wanaotoa maoni yao, mamlaka za Burkina Faso zinapaswa kufungua nafasi kwa mashirika ya kiraia, kuheshimu uhuru wa kujieleza, na kuondoa marufuku ya shughuli za vyama vya siasa," amesisitiza.
Chanzo; Nipashe