Kundi la M23 linaripotiwa kusajili wanajeshi, kuwatoza wakaazi kodi na kuwapa mafunzo wanajeshi na maafisa wa polisi ili kufanikisha azma yao ya kuunda serikali ya kinzani. Serikali ya Kongo imezifunga benki na kusitisha huduma nyingine za msingi baada ya wafanyakazi wa umma kukimbia Mashariki mwa Kongo kutokana na mapigano.
Kwa mujibu wa kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Corneille Nangaa azma yao ni kuipindua serikali ya Rais Felix Tshisekedi na kuunda uongozi mpya unaojikita katika uwazi na utendaji.
Kibarua chao kikubwa ni kuwabadili wakaazi mawazo na kuwarai kuwa na imani nao. Katika miezi ya kwanza, M23 iliteua magavana, madiwani, waratibu na kuanza kutoa huduma za vitambulisho na hati za usajili.
Hata hivyo, miji mikubwa ya Goma na Bukavu ya majimbo ya Kivu ya Kaskazini na Kusini, haijakuwa na maafisa wa polisi wala mahakama zinazofanya kazi na hivyo kuwepo kwa ongezeko la visa vya uhalifu wanasema mashuhuda. Kufungwa kwa benki na mifumo ya biashara pia vimevuruga uchumi ambao tayari umedorora.
Duru zinaeleza kuwa tangu Agosti mwaka huu, M23 wametangaza mabadiliko kadhaa na kuchapisha video inayowaonyesha kikosi cha maafisa wake wapya wa polisi kilichojumuisha maafisa wa serikali wa zamani waliokamatwa wakati wa mashambulizi na wengine wapya.
Haijabainika iwapo walijiunga kwa hiari au kushinikizwa. Lengo la video hiyo ni kuusisitizia umma kuwa wamejipanga na kuajiri wataalamu kinyume na hali ilivyo kwenye kikosi cha taifa ambacho kimechafuliwa na madai ya ufisadi. M23 pia imeandaa mtihani wa mchujo kwa ajili ya wanasheria wapatao 500 watakaowajumuishwa kwenye idara ya mahakama.
Kulingana na ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa ya Julai, kundi hilo limekuwa likiendesha operesheni zake za uongozi pasina vigezo vya msingi vya kisheria au mbinu za uwajibikaji hali inayozua adhabu na mauaji ya kiholela.
Ijapokuwa watuhumiwa wamefanyiwa msako ili kupunguza viwango vya uhalifu, mashirika ya kimataifa yanalalamika kuwa matokeo yake ni ukiukaji wa haki.
Ufadhili wa kundi la M23 bado unazua hisia mseto kwani mfumo wa benki umeporomoka Kongo. Kwa mujibu wa Reagan Miviri, mtaalam wa utafiti katika taasisi ya Ebuteli ya Kongo, M23 inahitaji msaada wa kigeni kwani operesheni za kijeshi zinazoendelea zinahitaji ufadhili mkubwa.
Ili kufidia pengo hilo la benki M23 imeunda mamlaka ya fedha ya kukusanya mapato, kutenga kodi maalum za biashara na uchimbaji wa madini.
Hata hivyo wakaazi wanalalamika kuwa hawana chochote na wanashurutishwa kulipa kodi katika mazingira magumu ya vita Mwezi uliopita, chama kikuu cha wafanyakazi jimboni Kivu ya Kusini kiliwasilisha ujumbe kwa M23 kuwaomba wapate msamaha wa kodi kwani wanasakamwa na madhila ya vita.
Chanzo; DW