Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Ali Mwadini amesema lugha ya Kiswahili sasa itatumika kama lugha rasmi katika Mikutano ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) baada ya kupitishwa kwa sauti moja.
Kwa mujibu wa balozi Mwadini, hatua hiyo ya kihistoria kwa lugha ya Kiswahili, imefikiwa leo Jijini Samarkand, Uzbekistan, ambako Mkutano Mkuu wa UNESCO unaendelea, kufuatia pendekezo lililowasilishwa na Tanzania, mapema mwaka huu.
Imeelezwa kuwa uamuzi huo uliofanya wakati wa kikao cha UNESCO cha 43 huko Uzbekistan, unakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya kiafrika kufikia hadhi hiyo ndani ya shirika hili la kimataifa.
“Ninayo furaha ya kuwaletea habari njema ya kupitishwa kwa sauti moja, Azimio la Mkutano Mkuu wa UNESCO la kuitambua lugha ya Kiswahili kama moja ya lugha rasmi za Mkutano Mkuu wa UNESCO,” amesema Balozi Mwadin.
Chanzo; Nipashe