Mji wa Moscow uliandaa kikao cha kwanza cha Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026, tukio linalotekelezwa chini ya mradi wa kitaifa wa “Vijana na Watoto.” Kwa mujibu wa agizo lililosainiwa na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, tamasha hilo kubwa la kimataifa litafanyika katika mji wa Ekaterinburg mnamo Septemba 2026.
Kamati ya Maandalizi inaongozwa na Naibu Mkuu wa Kwanza wa Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi, Sergei Kiriyenko, na inajumuisha wawakilishi wa Ofisi ya Rais na Serikali ya Urusi, mamlaka za shirikisho, viongozi wa makampuni makubwa ya Urusi, wakuu wa vyuo vikuu vinavyoongoza, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya habari na vyombo vya habari vya Urusi.

Akizungumza katika kikao hicho, Sergei Kiriyenko alisema kuwa Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 litawakutanisha vijana 10,000 kutoka nchi 190 duniani kote. Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza, ujumbe wa washiriki kutoka nje ya nchi utaandaliwa kulingana na nyanja zao za shughuli na utausisha vijana bora kutoka sekta za ubunifu, utawala wa umma, sayansi na teknolojia, michezo, ujasiriamali, vyombo vya habari na sekta ya kijamii.
“Ni muhimu sana kwa Tamasha hili kuwa jukwaa la kuonesha miradi na mifano bora ya Urusi. Tunataka kuonesha Urusi halisi—nchi yenye fursa zisizo na kikomo, ambapo watu wanaweza kuota ndoto na kuzitimiza. Kauli mbiu ya Tamasha la 2026, ‘Fuata ndoto yako. Pamoja na Urusi,’ inaakisi dira hiyo. Katika Mwaka wa Umoja wa Watu wa Urusi, uliotangazwa na Rais Vladimir Putin, Tamasha hili litakuwa tukio la kuunganisha watu, likionesha utajiri, utofauti na upekee wa tamaduni za mataifa ya Urusi,” alisema Kiriyenko.

Kamati pia ilipendekeza kuendeleza mpango wa safari za kikanda kwa washiriki wa kigeni katika mikoa 30 ya Urusi, kwa lengo la kuwaonesha maisha halisi ya nchi hiyo, urithi wake wa kitamaduni na historia ya karne nyingi ya kuishi kwa amani kwa mataifa mbalimbali. Kwa mara ya kwanza, safari moja ya kimataifa pia itaandaliwa katika nchi rafiki yenye uhusiano wa kihistoria na kitamaduni na Urusi Jamhuri ya Abkhazia.
Naibu Waziri Mkuu wa Shirikisho la Urusi na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Dmitry Chernyshenko, alisisitiza kuwa kuandaa Tamasha hilo Ekaterinburg ni jukumu kubwa, hasa baada ya mafanikio ya Tamasha la Vijana Duniani 2024 lililofanyika katika kituo cha Sirius.
Alieleza kuwa Tamasha hilo litafanyika kuanzia Septemba 11 hadi 17, 2026, na litahusisha washiriki 5,000 kutoka Urusi (ikiwemo watoto 1,000 wenye umri wa miaka 14–17) pamoja na washiriki 5,000 kutoka nje ya nchi. Aidha, wanavolontia 2,000 watashiriki katika maandalizi na utekelezaji wa tukio hilo.

Mkurugenzi wa Shirika la Shirikisho la Masuala ya Vijana (Rosmolodezh) na Katibu Mtendaji wa Kamati ya Maandalizi, Grigory Gurov, aliwasilisha dhana ya awali ya Tamasha hilo, akisisitiza kuwa lengo ni kuifanya Ekaterinburg kuwa “Mji wa Vijana wa Dunia,” ambapo kutakuwa na programu za kielimu, matukio ya kitamaduni, tamasha na maonesho mbalimbali katika jiji zima.
Ripoti kuhusu utayari wa miundombinu ya Mkoa wa Sverdlovsk zilitolewa na Gavana wa mkoa huo, Denis Pasler, pamoja na Waziri wa Sayansi na Elimu ya Juu wa Urusi, Valery Falkov, aliyebainisha kuwa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Shirikisho la Ural itatumika kuwahifadhi washiriki wa Tamasha hilo.
Kikao hicho pia kilijadili masuala ya ufadhili na usalama wa tukio.
Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 linaandaliwa na Shirika la Shirikisho la Masuala ya Vijana (Rosmolodezh), huku World Youth Festival Directorate likiwa mwendeshaji rasmi wa tukio hilo.