Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amepinga vikali hujuma ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela, akisema hatua hiyo inakiuka kanuni za Umoja wa Mataifa, kudhoofisha uhuru wa nchi huru na kuhatarisha amani na usalama wa kimataifa.
Ramaphosa alitoa wito wa kuachiliwa kwa haraka Rais Nicolás Maduro na mkewe, akisisitiza kwamba mashambulizi ya upande mmoja ni kinyume na uhuru na mamlaka ya kujitawala ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Tayari Afrika Kusini imeomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lifanye mkutano maalum na kuchukua hatua madhubuti za kulinda misingi ya sheria ya kimataifa na kuzuia matumizi ya nguvu bila idhini sahihi.
Ramaphosa ameonyesha msimamo thabiti wa kutetea uhuru wa kitaifa na usalama wa dunia, akitoa mfano wa nchi kama Libya na Iraq ambapo uvamizi wa kijeshi ulisababisha mizozo na ukosefu wa utulivu.
Hii ni ishara kwamba dunia inapaswa kutafuta suluhu za kisiasa na kidiplomasia badala ya migogoro ya kijeshi.
Chanzo; Global Publishers