Mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Uganda, Bobi Wine, amesema kuwa endapo atashinda uchaguzi huo, atapitia upya mikataba ya mafuta iliyopo kati ya serikali ya Uganda na makampuni ya kimataifa, kwa lengo la kuhakikisha inalinda maslahi ya wananchi wa Uganda.
Uganda inajiandaa kuanza uzalishaji wa mafuta ghafi kwa ajili ya biashara baadaye mwaka huu, kupitia ushirikiano na makampuni ya TotalEnergies ya Ufaransa, CNOOC ya China pamoja na Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Uganda, chini ya makubaliano ya kugawana uzalishaji na serikali.
Akizungumza na Reuters katika mahojiano yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Kampala, Bobi Wine ambaye pia ni msanii maarufu wa zamani alisema mikataba yote itafanyiwa mapitio, na sehemu yoyote itakayobainika kutowanufaisha Waganda itarekebishwa.
Wine anatarajiwa kumenyana tena na Rais wa sasa Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye ameiongoza Uganda kwa takribani miaka 40. Katika uchaguzi wa mwaka 2021, Bobi Wine alipata asilimia 35 ya kura.
Uganda inakadiriwa kuwa na akiba ya mafuta ghafi ya mapipa bilioni 6.65, yaliyogunduliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Hata hivyo, uzalishaji wake umecheleweshwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokubaliana kati ya serikali na makampuni ya kimataifa pamoja na upinzani kutoka kwa wanaharakati wa mazingira.
Serikali ya Uganda imekuwa ikikabiliwa na tuhuma za kukandamiza haki za binadamu na wakosoaji wake, madai ambayo imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara.
Chanzo; Global Publishers