Ushindi wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa urais wa Uganda uliofanyika Januari 15, 2026, sasa unakabiliwa na mtihani wa kisheria baada ya kupingwa mahakamani na mgombea wa urais Robert Kasibante.
Kasibante, aliyeshika nafasi ya sita katika uchaguzi huo kupitia Chama cha National Peasants Party (NPP), amefungua pingamizi akidai uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki, akitaja kasoro kubwa ikiwemo kushindwa kwa vifaa vya kielektroniki vya utambuzi wa wapiga kura katika maeneo mengi.
Aidha, amedai Tume ya Uchaguzi haikutumia mifumo ya uwazi katika ukusanyaji na utangazaji wa matokeo, pamoja na udhibiti wa mawasiliano ya umma uliodhoofisha uhalali wa mchakato mzima.
Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi na Rais Museveni kupitia mawakili wake wamepinga madai hayo wakisisitiza kuwa uchaguzi ulifanyika kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi, na kuomba kesi hiyo itupiliwe mbali.
Mgogoro huo umejiri katika mazingira ya sintofahamu ya kisiasa yaliyogubikwa na madai ya ghasia, udhibiti wa wapinzani na kuzimwa kwa mtandao, huku macho ya wengi yakielekezwa mahakamani kusubiri hatima ya ushindi wa Museveni na mustakabali wa demokrasia ya Uganda.
Chanzo; Mwananchi