Watu 17 wamepoteza maisha na wengine 11 kujeruhiwa baada ya mvua kubwa pamoja na theluji ya kwanza ya msimu kusababisha mafuriko ya ghafla katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan.
Taarifa hiyo imethibitishwa na msemaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Majanga ya Afghanistan siku ya Alhamisi, akisema idadi hiyo huenda ikaongezeka kadiri taarifa zaidi zinavyoendelea kupokelewa kutoka maeneo yaliyoathirika.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mvua hizo kubwa zilinyesha baada ya kipindi kirefu cha ukame kilichodumu kwa miezi kadhaa, hali iliyoifanya ardhi kuwa kavu kupita kiasi.
Kutokana na hali hiyo, maji ya mvua hayakuweza kupenya ardhini kwa urahisi na badala yake yakasababisha mafuriko ya ghafla yaliyotiririka kwa kasi, yakisomba nyumba, mifugo na mali za wakazi.
Mikoa kadhaa, hususan ya vijijini na maeneo ya milimani, imeripotiwa kuathirika zaidi.
Nyumba nyingi zimeharibiwa au kusombwa kabisa na maji, mashamba ya kilimo yameathirika vibaya, na miundombinu muhimu kama barabara na madaraja imekatika.
Hali hii imefanya iwe vigumu kwa vikosi vya uokoaji kufika kwa haraka katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika.
Mamlaka ya Usimamizi wa Majanga imesema timu za uokoaji zimepelekwa katika maeneo husika kwa ajili ya kuwatafuta manusura, kutoa huduma ya kwanza kwa waliojeruhiwa na kusambaza misaada ya dharura, ikiwemo chakula, maji safi na malazi ya muda.
Serikali pia imeanza kufanya tathmini ya kina ili kubaini kiwango halisi cha uharibifu na mahitaji ya waathirika.
Aidha, wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa, hususan wale wanaoishi karibu na mito na maeneo ya mabonde.
Mamlaka imetoa onyo kuwa mvua zaidi zinatarajiwa katika siku zijazo, hali inayoongeza hatari ya kutokea kwa mafuriko mengine.
Wataalamu wameeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuifanya Afghanistan kukabiliwa na majanga ya asili mara kwa mara, ikiwemo ukame mkali unaofuatwa na mafuriko makubwa.
Chanzo; Global Publishers