Serikali ya Kenya imesema itafanya mazungumzo na Urusi kufuatia ripoti zinazoongezeka kuwa raia wa Kenya wanasajiliwa kupigana vita nchini Ukraine, hatua ambayo imeitaja kuwa haikubaliki.
Shinikizo limeendelea kuongezeka kwa serikali kuchukua hatua, baada ya kugunduliwa kwa miili zaidi ya raia wa Kenya waliodaiwa kusajiliwa kupigana pamoja na vikosi vya jeshi la Urusi dhidi ya Ukraine.
Mamlaka za Kenya zinasema raia wanane waliokuwa wamesafiri kwenda Urusi wamefariki na bado hawajulikani walipo, huku taarifa zikionyesha kuwa watu wengine bado wanaendelea kujiunga na kampeni hiyo ya usajili.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amesema mazungumzo na Moscow yatalenga kudhibiti na kupunguza vitendo vya kusajili raia wa Kenya kinyume cha sheria. Pia najadiliano hayo yatahusisha masuala ya utoaji wa visa na makubaliano ya ajira kati ya nchi hizo mbili.
Mudavadi ameongeza kuwa makubaliano rasmi ya ajira kati ya Kenya na Urusi yataainisha wazi maeneo halali ya ajira ili kuhakikisha uwazi na ulinzi wa raia, akisisitiza kuwa Wakenya hawapaswi kuingizwa au kusajiliwa katika jeshi la Urusi.
Chanzo; Crown Media