Mamadou Diallo akamatwa na polisi kwa kuwauzia watu magari kupitia Facebook kisha kuyaiba tena na huenda akabiliwa na kifungo cha miaka 98 jela
Mamadou Diallo ambaye ni raia wa Missouri Marekani amekamatwa kwa tuhuma za kuendesha mpango wa utapeli uliowahusisha wanunuzi wa magari kupitia Facebook Marketplace.
Kwa mujibu wa polisi, Diallo alikuwa akiuza magari kwa wanunuzi anaokutana nao ana kwa ana na kuwapatia hati za umiliki (titles) na mikataba ya mauzo (bills of sale) zinazoonekana kuwa halali.
Hata hivyo muda mfupi baada ya miamala kukamilika alikuwa akiyarudisha magari hayo kwa wizi.
Diallo mwenye umri wa miaka 24 sasa anakabiliwa na mashtaka 14 ya jinai nzito (felony) baada ya kuwatapeli angalau waathiriwa 8 akiwapora zaidi ya dola 24,000 sawa na Milioni 61.3 kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Kaunti ya Jackson, Melesa Johnson, aliyetoa taarifa hiyo Alhamisi.
Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha kuwa Diallo anakabiliwa na mashtaka 6 ya kumiliki gari kinyume cha sheria na mashtaka 8 ya kughushi nyaraka (forgery).
Iwapo atapatikana na hatia kwa mashtaka yote, Diallo anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 98 jela.
Chanzo; Bongo 5