Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Jana Jumatano amesema kwamba hatua ya Marekani kususia mkutano wa G20 utakaofanyika Afrika Kusini mwishoni mwa mwezi huu haitazuia kikao cha uchumi mkubwa duniani kuendelea.
“Tutafanya maamuzi ya msingi na kutokuwepo kwao ni hasara yao,” Ramaphosa aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa Washington inakwepa “jukumu muhimu sana ambalo wanapaswa kulitekeleza kama taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani,” kwa mujibu wa AFP.
Rais wa Marekani, Donald Trump, awali alitangaza kuwa hakuna maafisa wa Marekani watakaohudhuria mkutano wa G20, akitaja sababu kuwa ni jinsi Afrika Kusini inavyowatendea wakulima weupe.
“Ni fedheha kubwa kwamba G20 itafanyika Afrika Kusini,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social. Utawala wa Trump kwa muda mrefu umekuwa ukishutumu serikali ya Afrika Kusini kwa ubaguzi dhidi ya wachache weupe, ukieleza madai ya kunyang’anywa ardhi na matukio ya vurugu.
Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai kwamba Waafrika Kusini kutoka jamii ya kizungu (Afrikaners) au wazungu wengine nchini humo wanateswa.
Chanzo; Dw