Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema umefika wakati kwa mataifa ya Afrika kujiimarisha kiusalama na kujihami bila kuacha hatima ya bara hilo iamuliwe na mataifa ya nje.
Amesema Afrika ina uwezo wa kujisimamia kikamilifu endapo itatumia vyema rasilimali zake na kuimarisha mshikamano wa kikanda.
Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi, Februari 7, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam, Museveni amesema kwa muda mrefu mataifa ya Afrika yamekuwa yakikosa mikakati madhubuti ya kujilinda dhidi ya ushawishi na vitisho kutoka nje, hali iliyochangia kuyumbisha uwezo wa nchi hizo kufanya maamuzi huru kwa maslahi yao.
“Hatuna sababu ya kuogopa mataifa ya nje kuamua mustakabali wetu ilhali tuna rasilimali za kutosha na uwezo wa kujisimamia. Tunachohitaji ni umoja na dhamira ya pamoja,” amesema Rais Museveni.
Amesema njia sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo ni Waafrika kuungana kidiplomasia na kiuchumi, hatua itakayowezesha bara hilo kuwa na nguvu ya pamoja na sauti moja katika kulinda masilahi yake ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi.
Chanzo; Mwananchi