Rais wa zamani wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ya uchochezi na uasi.
Mahakama ya Wilaya ya Seoul Central imetoa uamuzi huo leo Alhamisi Februari 19, 2026, ambao ulitangazwa moja kwa moja kwa umma kupitia vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti mahakamani hapo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kiini cha kesi ya sheria ya kijeshi dhidi ya Yoon kilikuwa ni ukweli na kwamba wanajeshi walipelekwa katika Bunge la Taifa.
Timu ya Cho Eun-suk, wakili huru aliyekuwa akisimamia kesi ya uasi wa Yoon na makosa mengine yanayohusiana, iliomba hukumu ya kifo kwa Yoon kwa mashtaka ya kupanga uasi kwa kutangaza hali ya hatari ya sheria ya kijeshi isiyo ya kikatiba na isiyo halali licha ya kutokuwapo kwa vita, tukio au dharura nyingine ya kitaifa inayolingana na hiyo.
Mahakama ilieleza kuwa tangazo la sheria ya kijeshi linachukuliwa kuwa uasi iwapo linakiuka mamlaka ya Bunge la Taifa, ikibainisha kwamba Yoon alijaribu kuzuia bunge kufanya kazi ipasavyo kwa muda mrefu.
Chanzo; Mwananchi