Ajali mbaya ya baharini imesababisha vifo vya watu 11 baada ya boti iliyokuwa imebeba watu wa jamii wa Rohingya kutoka Myanmar kuzama karibu na mpaka wa bahari wa Thailand na Malaysia.
Tukio hilo lilithibitishwa na mamlaka za pande zote mbili Jumatatu, Novemba 10, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Usalama wa Baharini la Malaysia (MMEA), boti hiyo iliondoka kutoka pwani ya Myanmar siku chache kabla ya ajali na ilikadiriwa kubeba takriban watu 70 waliokuwa wakielekea Malaysia kupitia Bahari ya Andaman.
Mamlaka zinasema kuwa boti hiyo ilipata dhoruba kali na mawimbi makubwa yaliyopelekea kupinduka, na kusababisha abiria wengi kutoweka baharini.
Hadi sasa, jumla ya watu 11 wamethibitishwa kufariki dunia, wakiwemo watoto wawili.
Miili minne ilipatikana upande wa Thailand, huku mingine ikipatikana katika maji ya Malaysia.
Aidha, watu 13 waliokolewa wakiwa hai, miongoni mwao wakiwa 11 ni wa jamii ya Rohingya na wawili ni raia wa Bangladesh.
Wote wamepelekwa kwenye vituo vya afya na wanapatiwa huduma na uchunguzi wa uhamiaji.
Oparesheni kubwa ya uokoaji inaendelea kuongozwa na majeshi ya baharini ya Thailand na Malaysia, yakishirikiana na vikosi vya anga.
Eneo la uokoaji linakadiriwa kufikia zaidi ya kilomita za mraba 400, huku mamlaka zikiahidi kuendelea na juhudi hizo kwa angalau siku saba.
Mamlaka za Thailand zimeripoti pia uwepo wa boti nyingine iliyokuwa na zaidi ya watu 230 ambayo haijulikani ilipo hadi sasa, na hofu imeongezeka kuwa inaweza pia kuwa imezama.
Mashirika ya haki za binadamu yameelezea masikitiko yao na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzuia vifo zaidi ya aina hii.
Tukio hili linaangazia tena mateso na hatari kubwa zinazowakabili watu wa jamii ya Rohingya, ambao wamekuwa wakikimbia mateso na hali mbaya katika jimbo la Rakhine, Myanmar, na kwenye kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 5,000 wa Rohingya wamejaribu kusafiri baharini kuelekea nchi za Asia ya Kusini Mashariki mwaka huu pekee, huku takriban 600 wakihofiwa kufariki au kupotea baharini.
Chanzo; Global Publishers