Tukio la kutisha limeripotiwa katika jimbo la Jharkhand, mashariki mwa India, ambako mwanamke mmoja na mtoto wake wa miezi 10 wameuawa kwa kuchomwa moto hadi kufa baada ya kutuhumiwa kuwa wachawi.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, kundi la watu lilivamia nyumba ya familia hiyo mapema wiki hii na kuwashambulia kwa madai kwamba mwanamke huyo alikuwa akijihusisha na uchawi.
Mume wa mwanamke huyo, ambaye pia alilengwa katika shambulio hilo, alipata majeraha mabaya ya moto na kwa sasa amelazwa hospitalini akipokea matibabu.
Tuhuma za uchawi zimekuwa chanzo cha ukatili katika baadhi ya maeneo nchini India, hasa katika majimbo ya mashariki na kati.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu za Uhalifu, zaidi ya watu 2,500, wengi wao wakiwa wanawake, waliuawa nchini India kwa tuhuma za uchawi kati ya mwaka 2000 na 2016.
Chanzo; Dw