Mahakama Nchini China imewahukumu kifo Watu 11 wa familia moja kwa kosa la kuendesha mtandao mkubwa wa uhalifu ulioshirikisha kamari haramu, ulaghai wa mtandaoni na mauaji ambapo kiasi cha fedha kinachohusishwa na uhalifu huo kinakadiriwa kuzidi dola za kimarekani ambazo ni zaidi ya trilioni 3 za Kitanzania.
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya kati ya Jimbo la Wenzhou Jumatatu ya Septemba 29 ambapo miongoni mwa waliohukumiwa ni Ming Guoping, Ming Zhenzhen, na Zhou Weichang ambao wote wa familia moja yenye ushawishi katika eneo la Kokkang, Myanmar.
Aidha, Mahakama pia ilitoa hukumu ya kunyongwa kwa Watu wengine watano adhabu ya kifo iliyosimamishwa kwa miaka miwili ambayo mara nyingi hubadilishwa kuwa kifungo cha maisha, huku Washtakiwa 12 wakipata vifungo vya kati ya miaka mitano na 24.
Mnamo Novemba 2023, China ilitoa hati ya kukamatwa kwa familia ya Ming kwa tuhuma za ulaghai, mauaji, na kuweka Watu kizuizini kinyume cha sheria ambapo upelelezi ulionyesha kuwa mtandao wao wa uhalifu uliendesha vituo vya ulaghai wa mtandaoni karibu na mpaka wa China na Myanmar.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mahakama uhalifu huo ulisababisha vifo vya Wafanyakazi 10 na kujeruhiwa kwa wengine wawili waliojaribu kutoroka katika Vituo hivyo huku Waathiriwa wakilazimishwa kushiriki katika ulaghai wa kimtandao.
Chanzo; Millard Ayo