Benki Kuu ya Kenya (CBK) imepiga mafukuru tabia ya wafanyabiashara kutumia noti za fedha kutengeneza mashada ya maua ya mapambo kuelekea Valentine Day, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi hiyo.
Mtindo huo, uliobuniwa na watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii, unahusisha kukunja na kufunga noti za fedha ili kupata mwonekano wa mashada ya maua ili wayauze kwa gharama.
Taarifa iliyotolewa na benki kuu hiyo, imesema kuwa kitendo hicho kinaharibu” fedha na kudhoofisha uhalali na uimara wa noti. Imeeleza kuwa watakaopatikana na hatia ya kuharibu fedha wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka saba jela.
Benki hiyo imefafanua kuwa noti zinazotumiwa kutengeneza mashada ya maua mara nyingi hugandishwa kwa gundi, kushonwa kwa viungio (staples), au kuchomwa kwa sindano.
Uharibifu huo husababisha noti hizo kushindwa kutumika kwenye mashine za ATM na mashine za kuhesabu fedha, hali inayosababisha “gharama zisizo za lazima” kwa umma na benki katika kuzibadilisha.
Chanzo; Mwananchi