Watu 15 wamekufa kufuatia ajali ya kugongana kwa mashua ya walinzi wa pwani ya Ugiriki na ile ya wahamiaji kando ya ufukwe wa kisiwa cha Chios, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka za Ugiriki jioni ya jana.
Hadi sasa, miili 15 ndiyo iliyoopolewa, yote ikiwa ya wahamiaji, alisema naibu meya Pantelis Vroulis, kwenye televisheni ya Ugiriki.
Televisheni hiyo, ERT, ilitangaza kuwa watu 25 wamepelekwa kwenye hospitali ya kisiwa hicho, kumi na moja wakiwa watoto wadogo na wawili wakiwa maafisa wa kikosi cha ulinzi wa pwani.
Vyombo vya habari vinasema watu kadhaa walikuwamo kwenye mashua hiyo ya wahamiaji iliyokuwa ikitokea Uturuki kuelekea Kisiwa cha Chios.
Sababu ya ajali hiyo inatajwa ni pale mashua ya walinzi wa pwani ilipojaribu kuikamata mashua ya wahamiaji na kuilazimisha kugeuza njia.
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, kiasi cha wahamiaji 1,000 wameingia kwenye visiwa vinavyotawaliwa na Ugiriki kwenye Bahari ya Aegan wakitokea Uturuki tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Chanzo; Dw