Rais wa Marekani Donald Trump na Washauri wake wameanza majadiliano mazito yanayoashiria uwezekano mkubwa wa kufikia maamuzi ya Marekani kutumia Jeshi lake kuchukua udhibiti wa kisiwa cha Greenland wakisema watakichukua kisiwa hicho kwasababu za kiusalama kwakuwa eneo hilo limejaa meli za Urusi na China.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, amesema Rais anao wajibu wa kuidhinisha Jeshi kufanya oparesheni mbalimbali ikiwemo hiyo ya kuchukua Greenland endapo ataona inafaa.
Kumezuka hali ya wasiwasi na ukosoaji Barani Ulaya kufuatia vitisho vya rais Donald Trump kwamba Marekani itachukua udhibiti wa eneo la Greenland lenye utajiri wa madini na lililopo chini ya himaya ya Denmark.
Viongozi wa Denmark na wale wa kisiwa cha nchi hiyo kinachojitawala chenyewe cha Greenland wamesisitiza kuwa Marekani kamwe haitoichukua Greenland na kuitaka Marekani kuheshimu hadhi ya mipaka inayotambuliwa kimataifa.
Trump amenukuliwa mara kadhaa akisema kwamba angetamani Marekani ikinyakue kisiwa hicho kwa sababu za kiusalama, ingawa mara zote kauli hizo zimeleta ukosoaji mkubwa kutoka kwa Denmark na Mataifa mengine hususani ya Ulaya.
Marekani tayari ina kambi ya kijeshi nchini Greenland, inayojulikana kama Kituo cha Anga cha Pituffik lakini Trump ameonesha nia ya kutaka udhibiti wa kisiwa chote akisema ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani, akidai kuwa eneo hilo limejaa meli za Urusi na China.
Greenland, kisiwa kikubwa cha Aktiki kilicho sehemu ya Ufalme wa Denmark, kiko takribani kilomita 3,200 kaskazini-mashariki mwa Marekani, kina utajiri mkubwa wa madini adimu yanayotumika katika teknolojia za kisasa, zikiwemo smartphone, magari ya umeme na vifaa vya kijeshi, kwa sasa, uzalishaji wa madini hayo nchini China unazidi kwa mbali ule wa Marekani
Chanzo; Millard Ayo