Shirika la kimataifa la Polisi wasio na mipaka la INTERPOL, limesema Vyombo vya sheria kutoka Nchi 16 za Afrika vimewakamata Washukiwa 651 na kurejesha zaidi ya dola za Marekani milioni 4.3 katika operesheni kubwa dhidi ya uhalifu wa mtandaoni unaovuka mipaka katika swala la utapeli wa kifedha.
Katika taarifa iliyotolewa na INTERPOL Jumatano Februari 19, 2026 ilieleza kuwa operesheni hiyo iliyopewa jina la Operation Red Card 2.0 ilidumu kwa wiki nane kuanzia Desemba 8, 2025 hadi Januari 30 mwaka huu ambapo ililenga kuwakamata Matapeli wa uwekezaji wenye ahadi za faida kubwa, wezi wa fedha kupitia mitandao ya simu pamoja na programu bandia za mikopo ya simu.
Katika kipindi hicho cha wiki nane, uchunguzi ulifichua ulaghai uliosababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 45, na Waathirika 1,247 waliotambuliwa ambapo wengi wao walitoka barani Afrika, huku wengine wakitoka maeneo mbalimbali duniani.
Aidha, Mamlaka zilitaifisha vifaa 2,341 na kuzima anuani 1,442 za IP, tovuti na seva zilizokuwa zikitumika kwa shughuli za kihalifu, pamoja na miundombinu mingine inayohusiana na uhalifu huo ambapo baadhi ya Nchi zilizoshiriki katika operesheni hiyo ni Angola, Cameroon, Côte d’Ivoire, Kenya, Nigeria na Zimbabwe, Benin, Cameroon, Gabon, Gambia, Ghana, Uganda, Zambia na Chad.
Chanzo; Millard Ayo