Mfanyabiashara mmoja kutoka Uingereza amehukumiwa kifungo cha miaka minne na miezi minane jela baada ya kukiri kuuza vipuri bandia vya injini za ndege vyenye thamani ya dola milioni 9.4 (takribani shilingi bilioni 24.1) kwa mashirika ya ndege na kampuni za matengenezo duniani.
Mahakama ilielezwa kuwa zaidi ya vipuri 60,000 vilivyouzwa vilikuwa vya kughushi na vikiambatanishwa na nyaraka za usalama zilizoghushiwa ili kuonekana halali na salama kwa matumizi katika ndege za abiria.
Mfanyabiashara huyo aliendesha biashara kupitia kampuni ya AOG Technics Ltd iliyokuwa ikisambaza vipuri mbalimbali vya injini ikiwemo blade, bolti, seal na washer.
Waendesha mashtaka walieleza kuwa kampuni hiyo ilitoa vyeti bandia vya uthibitisho wa ubora (safety certificates) ili kuvifanya vipuri hivyo vionekane kuwa vimeidhinishwa rasmi.
Sakata hilo lilifichuliwa Agosti 2023 baada ya wahandisi kugundua kuwa kifaa kimoja hakikutoshea ipasavyo wakati wa ukaguzi wa kawaida wa matengenezo.
Uchunguzi zaidi uliofanywa kwa kushirikiana na mtengenezaji halisi wa vipuri ulithibitisha kuwa nyaraka zilizoambatanishwa zilikuwa za kughushi.
Ugunduzi huo ulisababisha uchunguzi wa haraka kutoka kwa mamlaka za usafiri wa anga nchini Uingereza, Marekani na Ulaya na kusababisha tahadhari za kiusalama pamoja na ukaguzi maalum kwa ndege kadhaa.
Mashirika yaliyoathirika yalijumuisha American Airlines na Ethiopian Airlines ingawa hakuna ajali wala majeruhi walioripotiwa kuhusishwa na vipuri hivyo.
Baadhi ya ndege zililazimika kusimamishwa kwa muda kwa ajili ya ukaguzi na kubadilisha vipuri vinavyotiliwa shaka jambo lililosababisha hasara kubwa kifedha na usumbufu wa ratiba za safari.
Katika hukumu yake, jaji alieleza kuwa udanganyifu huo uliathiri mifumo ya udhibiti iliyoundwa kulinda abiria na kudumisha imani katika sekta ya anga.
Mbali na kifungo hicho, mfanyabiashara huyo amepigwa marufuku kuwa mkurugenzi wa kampuni kwa kipindi cha miaka minane na mamlaka zikianza mchakato wa kurejesha fedha alizopata kupitia mpango huo haramu.
Chanzo; Global Publishers