Mahakama nchini Tunisia imemuachilia huru leo Saber Chouchane, mwanamume mwenye umri wa miaka 56, ambaye wiki iliyopita alikuwa amehukumiwa kifo kwa kuchapisha kauli za kumkosoa rais.
Kuachiliwa kwa Saber Chouchane kumetokea baada ya wimbi la ukosoaji wa umma na wasiwasi kuhusu haki za binadamu uliotokana na kesi hiyo.
Wakili wake, Oussama Bouthelja, amethibitisha kuachiliwa kwa mteja wake, huku nduguye Saber, Jamal Chouchane, pia amethibitisha taarifa hiyo bila kutoa maelezo zaidi.
Uamuzi wa awali wa kumhukumu kifo ulionekana kuwa wa kipekee katika historia ya Tunisia, taifa ambalo limekuwa likikabiliwa na ongezeko la vizuizi dhidi ya uhuru wa kujieleza tangu Rais Kais Saied alipojilimbikizia mamlaka makubwa mwaka 2021.
Makundi ya kijamii na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu walielezea hukumu dhidi ya Saber kuwa ya kushangaza, na iliibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhuru wa maoni na haki za raia.
Chanzo; Dw