Zikiwa zimesalia siku 12 uchaguzi ufanyike Uganda, Rais Yoweri Museveni amedai kuwa mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amepanga ghasia akisaidiwa na wafadhili wake wa kigeni wasioitakia Uganda mema.
Katika hotuba yake ya mwaka mpya kwa taifa, rais Museveni amemtaja mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi kama mtu ambaye hajakomaa kisiasa na ndiyo maana hazingatii matokeo ya matamshi yake.
Kiongozi huyo ambaye ametawala Uganda kwa miaka 40 sasa anakosoa mataifa ya kigeni ambayo yanafadhili kampeni za Bobi Wine akielezea kuwa hayana nia njema kwa Uganda.
Kwa upande wake Bobi Wine amemjibu Museveni akisema kuwa ni wazi kwamba utawala wa Museveni ndiyo umejiandaa kuvuruga uchaguzi kutokana na kanuni ambazo zinazidi kutolewa kama vile kuwakataza watu kubaki kwenye vituo vya kupigia kura kufuatilia zoezi hilo kwa karibu.
Msimamo huo wa utawala anaulezea kuwa hila ya kuweza kughushi matokeo na hii inawatishia wapigajikura kuhusiana na kushiriki katika uchaguzi.Katika kipindi cha kampeni, polisi wameshuhudiwa wakiwacharaza wafuasi wa upinzani hasa wa chama kikuu cha upinzani cha NUP wakiwa kwenye misafara na mikutano ya kampeni.
Museveni amewahimiza kutotumia mbinu hiyo akiwashauri kutumia mabomu ya kutoa machozi lakini pia kwa tahadhari.
Chanzo; Nipashe