Mshukiwa wa gaidi ambaye alikwepa shirika la upelelezi la Marekani, FBI, kwa zaidi ya miaka 20 kabla ya kukamatwa huko Wales alifikishwa mahakamani mapema mweizi Septemba kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi ya kurejeshwa nchini humo.
Mtu anayeshukiwa kutekeleza mashambulizi mawili ya mabomu katika eneo la San Francisco nchini Marekani mwaka 2003 alikuwa kwenye orodha ya watu wanaotafutwa zaidi na FBI.
FBI wanaamini kuwa Daniel Andreas San Diego ana uhusiano na makundi ya itikadi kali za haki za wanyama na ndiye mshukiwa wao mkuu wa msururu wa mashambulizi ya mabomu katika eneo la Ghuba ya San Francisco mwaka 2003.
Maafisa wa zamani wa FBI wamesema "kulikuwa na fursa" za kumkamata mtu huyo mwenye umri wa miaka 47 kabla hajatoweka na kudai walipata "kiwanda cha kutengeneza mabomu" kinachoshukiwa kuwa ndani ya gari lake lililotelekezwa baada ya kile wapelelezi walichokiita msako wa mwendo wa maili 65 (104km) huko California. Bw. San Diego alipatikana kilo mita 8,000 sawa na (maili 5,000) kaskazini mwa Wales mwaka jana.
Kesi dhidi ya Bw San Diego, ambaye zawadi ya $250,000 pesa taslimu ilitolewa kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake, ilisikilizwa kwa siku tano katika mahakama ya Westminster mjini London ili kuamua ikiwa Uingereza itamuwasilisha kwa Marekani kujibu mashtaka baada ya waranti ya kukamatwa kwake kutolewa.
Kundi la watu wenye msimamo mkali wa kutetea haki za wanyama linalofahamika kama Animal Liberation Brigade lilidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya makampuni ambayo waliamini yana uhusiano na mashirika ambayo yalifanyia majaribio bidhaa za wanyama.
Aliyekuwa jasusi Maalum wa FBI David Smith alikuwa sehemu ya kikundi maalum cha oparesheni ambacho kimekuwa kikimfuatilia Bw San Diego.
"Alikuwa mtu wa ajabu sana," Bw Smith, mmoja wa wataalam wa ngazi ya juu wa wa FBI, aliiambia BBC.
"Alikuwa mdogo na mtu wa kawaida, hakuna kitu chochote kilichoashiria kuwa ni mtu hatari. Hakuonyesha dalili yoyote kwamba alikuwa anatufahamu."
Majasusi wa FBI walihisi kuwa wamepata maelezo ya kutosha kuthibibitisha kuwa Bw San Diego ndiye mshukiwa wake mkuu na walidhani ndiye alitega vifaa vilivyolipuka kwa mwezi mmoja.
Lakini jasusi maalum Andrew Black, ambaye alikuwa sehemu ya timu ya maafisa wa FBI ya kukabiliana na ugaidi, alikumbuka: "Ofisi ya Mwanasheria wa Marekani na maajenti wa kesi walikuwa wakifanya uamuzi wa iwapo akamatwe au waendelee kufanyia kazi mpango wao.
"Tulikuwa na matumaini mpango huo ungetuongoza kwa wanachama wengine wa kundi hilo la haki za wanyama ambalo limekuwa likitumia vurugu kukuza ajenda zao."
Mabomu mawili yalilipuka katika shirika la teknolojia ya kibayoteknolojia huko Emeryville, karibu na Oakland, Marekani, tarehe 28 Agosti 2003, huku wachunguzi wakiamini kuwa bomu la pili lilitegwa kuwalenga wahusika wa kwanza.
Kisha bomu lililokuwa ambalo lilikuwa limefungwa kwa misumari lililipuka katika kampuni ya bidhaa za lishe huko Pleasanton, maili 30 (48km) mashariki mwa kutoka kwa mlipuko wa kwanza, tarehe 26 Septemba 2003. Hakuna aliyejeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Wataalamu wa zamani wa uchunguzi wa FBI walifahamishwa kuwa Bw San Diego anaorodheshwa kama mshukiwa mkuu na kwamba walitakiwa kumfuatilia kwa karibu kwa sababu "kukamatwa kwake kunakaribia".
"Tulikuwa tukimfuatilia mtu ambaye tunafikiri amefanya mashambulizi mingi ya mabomu na gaidi wa nyumbani," alikumbuka Bw Smith.
Bw Smith na mwenzake wa zamani Clyde Foreman, aliyekuwa wakala maalum wa usimamizi, wanakumbuka waliwasihi wenzao wamtie mbaroni mara tu atakapotambuliwa kuwa mshukiwa mkuu.
Bw Black, ajenti aliyehudumu kwa miaka 27, aliongeza: "Kadiri uwezavyo kuwa mzuri, kudumisha ufuatiliaji hatimaye watagundua jambo lisilo la kawaida na kuingiwa na uoga.
"Kulikuwa hali ya sintofahamu kwa sababu hawakupewa ishara ya kumkamata kwani walihisi akiepuka mtego wao huenda akafanya mashambulizi zaidi ya mabomu."
Siku moja kabla ya San Diego kukwepa mtego wa FBI, Bw. alikuwa amejificha nje ya nyumba yake.
Saa chache baada ya Bw Smith na wataalamu wa uchunguzi wa FBI kukamilisha zamu, alisema Bw San Diego aliwakimbia wapelelezi kimya kimya.
"Tangu lipotoka nje ya nyumba yake, alikuwa akitenda kwa hasira," alikumbuka Bw Smith.
"Mtindo wake wa uendeshaji gari ulibadilika. Alikokuwa akienda, alikuwa akiendesha gari bila mpangilio jambo ambalo hufanywa na mtu anayejaribu kukwepa kufuatiliwa."
Maajenti wanasema alisafiri kuelekea kusini mwa nyumbani kwake huko Sebastopol, Kaunti ya Sonoma, akipitia barabara za chini kwa chini katika safari iliyomchukua saa moja kufika Francisco.
Hata ndege za kijasusi za FB pia zilishindwa kumfuatilia mshukiwa baada ya ukungu maarufu wa San Francisco kuwazuia kumuona Bw San Diego akitoroka mtego wao.
San Diego aliacha gari lake likiwa halijazimwa, kwenye makutano ya katikati ya jiji lenye shughuli nyingi karibu na kituo cha treni ya chini ya ardhi, na hakuonekana tena.
"Timu iliyomfuata ilikuwa ikifikiria kuwa aliegesha gari na kupita nyumba kadhaa kando ya barabarani na kuelekea hadi eneo la karibu, linalojulikana na kundi la kutetea haki za wanyama au alikuwa na uhusiano nalo," alikumbuka Bw Smith, mpelelezi wa FBI kwa miaka 33.
"Niliuliza 'kama kuna mtu yeyote aliyemuona akiingia au kutafuta namna ya kutoka mahali hapo muda mfupi uliopita?' Walijibu kuwa hawakuona.
"Gari liliegeshwa katika eneo la basi karibu na njia ya chini ya ardhi na tukasema 'pengine ameenda'. Bw. Foreman pia alifikiria hivyo.
"Tulifahamu fika kwamba yuko mbioni na itakuwa vigumu kumpata," alikumbuka.
"Wapelelezi waliendesha uchunguzi wao walidhani kuwa San Diego alikuwa akitumia makazi yake kutengeneza bomu lake.
"Alipotelekeza gari lake, tuligundua maabara yake ya kutengeneza bomu ilikuwa kwenye buti la gari lake."
Bwana Smith alitazama buti likifunguliwa na kuthibitisha alichokiona ni "kitu ambacho kila mpelelezi angetaka kukiona".
"Laiti tungelijua hilo, hakika angelikuwa amekamatwa kitambo," aliongeza.
"Ilikuwa sawa kutumia neno ilikuwa. Tulijiridhisha moj akwa moja huyu ndiye mtu tunayemsaka. Tulikuwa wapelelezi wenye uzoefu mkubwa na tulimfahamu mshukiwa tulipomwona.
"Kwa hakika ilikuwa ni fursa iliyotuponyoka."
Mashambulizi hayo mawili yalifanywa miaka miwili baada ya shambulio la 9/11 na Marekani ilikuwa katika hali ya tahadhari, hivyo mkuu wa idara Bw Foreman alitoa maelekezo kwamba: "Ukishamtambua mtu, mkamate."
Bw San Diego alikuwa mtaalamu wa mtandao wa kompyuta aliyezaliwa Berkeley, California, na alilelewa katika eneo la tabaka la kati la eneo la San Francisco Bay . Baba yake alikuwa msimamizi wa jiji.
FBI ilikuwa na kibarua cha kumtafuta Bw San Diego kwa miaka kadhaa baada ya bwana huyo kutoweka, ikishirikiana na jamaa na marafiki zake kuona kama wanaweza kuwaongoza maajenti kwake. Lakini hawakufanikiwa. Waliamini pengine alikimbilia Amerika ya kati au Kusini.
Bw San Diego alishtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani mwaka wa 2004 na FBI ilimchukulia mtu hatari na aliyejihami kwa silaha.
Baada ya miaka 21 Bw. Smith na Foreman walistaafu, walisikia kwamba mmoja wa washukiwa ambo wamekuwa wakiwatafuta kwa muda anazuiliwa nchini Uingereza baada ya kupatikana katika eneo lenye mlima huko Wales kaskazini.
Shirika la Kitaifa la kukabiliana na Uhalifu la Uingereza (NCA) na polisi wa kukabiliana na ugaidi walivamia Novemba 2024, na kumkamata Bw San Diego ambaye amekuwa akitumia jina la Danny Webb katika bonde la Conwy, karibu na mji wa soko wa Llanrwst.
"Naamini alikuwa akipata usaidizi - haumtafuti Jason Bourne," alisema Bw Foreman.
"Hakuwa afisa wa ujasusi mwenye ujuzi. Lazima alipata usaidizi kutoka mahali."
FBI ilisema haitatoa tamko lolote kuhusu uwezekano wa kukosa fursa za kumkamata Bw San Diego.
Lakini wakati wa kukamatwa kwake, Mkurugenzi wa FBI, Christopher Wray alisema: "Kukamatwa kwa Daniel San Diego baada ya kuwa mafichoni kwa zaidi ya miaka 20 kwa kuhusika na mashambulizi miwili ya mabomu katika eneo la San Francisco kunaonyesha kwamba haijalishi itachukua muda gani, FBI itakupata na kuwajibisha."
Bw San Diego, ambaye anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Belmarsh mjini London, amekataa kuzungumzia kile kinachomsibu.
Chanzo: Bbc