Rais wa Marekani Donald Trump, amesema wazi kuwa anaunga mkono Nchi za NATO kuzitungua Ndege za kivita za Urusi zitakazoingia kwenye anga zao bila kibali.
Trump ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na Rais Zelensky wa Ukraine, pembeni ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo jibu hilo lilitokana na swali la iwapo NATO inapaswa kuzishambulia ndege hizo.
Trump alijibu kwa haraka “Ndiyo, nafikiria hivyo”
Hata hivyo alipoulizwa kama Marekani itaingia kwenye hilo moja kwa moja, alisema itategemea na mazingira lakini akasisitiza kuwa Marekani ina msimamo imara ndani ya NATO.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo hali ya tahadhari imeshika kasi Barani Ulaya baada ya Ndege za kivita za Urusi aina ya MiG-31 kuingia kwenye anga ya Estonia, huku wiki iliyopita zikiripotiwa pia kuingia ndani ya anga ya Poland ambapo tayari baadhi ya Mataifa ya Ulaya yamesema iko wazi kuwa Ndege au drone yoyote ya Urusi ikivuka tena mipaka itaangushwa.
Chanzo; Millard Ayo