Mwanamuziki kutoka lebo wa WCB, Zuchu ameweka wazi kuwa hakulipwa pesa katika onyesho alilolifanya katika fainali za ‘CHAN 2024’. Onesho ambalo liliyofanyika Agosti 30,2025 jijini Nairobi, Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Zuchu amechapisha ujumbe wa wazi kwenda CAF akilalamika kutopokea malipo aliyostahili kwa utumbuizaji wake katika fainali za michuano hiyo.
“Natumai ujumbe huu umewafikia salama. Ninaandika kueleza wasiwasi na masikitiko yangu kuhusiana na malipo ambayo bado sijapokea kwa ajili ya onyesho langu la hivi karibuni lililofanyika Nairobi tarehe 30 Agosti 2025. Kwa mujibu wa makubaliano yetu na mawakala wenu kutoka LEAP Creative Agency, malipo yote ya huduma zangu yalitakiwa kulipwa mara tu baada ya tukio kukamilika, lakini licha ya mimi na timu yangu kuwa wavumilivu na wenye kuelewa hali hii kwa muda mrefu, bado sijapokea malipo kamili.
“Timu yangu ya usimamizi imekuwa ikiwasiliana mara kwa mara na wanachama mbalimbali wa shirika la LEAP ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Roshan Soomarshun, bila mafanikio. Hata hivyo, vielelezo vya malipo (POPs) vilivyodaiwa kutumwa viligeuka kuwa visivyo na uhakika, vya kutiliwa shaka na wazi kwamba havikutumwa wala kulipwa,”ameandika Zuchu
Hata hivyo hakuishia hapo ameendelea kwa kueleza kuwa “Nimekamilisha wajibu wangu ipasavyo kwa kutoa onyesho ambalo nilijitolea kikamilifu kuhakikisha linafikia viwango vya juu zaidi. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa kiwango sawa cha taaluma hakijatumika upande wenu katika kutimiza majukumu yenu ya kifedha,"ameandika