Baada ya maswali mengi kuhusu nani atatumbuiza katika jukwaa la Super Bowl Half Time Show 2026. Hatimaye NFL, Apple Music na Roc Nation Jumapili ya Septemba 28, 2025, wamemtangaza mwanamuziki na mwigizaji, Bad Bunny kuwa kinara kwenye shoo hiyo itayofanyika katika uwanja wa Levi Februari 8,2025, huko Santa Clara, California nchini Marekani.
Bad Bunny mwenye umri wa miaka (31) anaingia kwenye uteuzi huo wa Super Bowl akiwa msanii aliyeteuliwa katika vipengele vingi vya tuzo za Grammy za Kilatini zinazotarajiwa kufanyika Novemba, 2025 huku akiwa ni mmoja wa waigizaji katika filamu kama Bullet Train na Happy Gilmore 2.
Akiwa na jumla ya albamu 11 na Ep 2 kama vile Un Verano Sin Ti ya lugha ya Kihispania na albamu yake ya 2025, Debí Tirar Más Fotos, Bad Bunny ni mmoja wa wasanii wanaosikilizwa zaidi kwenye majukwaa ya muziki duniani.
"Ninachohisi kinapita zaidi yangu, ni kwa wale waliokuja kufanya kabla yangu ili niweze kuingia na mimi. Hii ni kwa ajili ya watu wangu, utamaduni wangu, na historia yetu," alisema Bunny katika taarifa yake akishukuru kuteuliwa kwenye Super Bowl.
Kutangazwa kwa Bunny Super Bowl 2026 kunakuja ikiwa ni wiki kadhaa baada ya msanii huyo, mzaliwa wa Benito Antonio Martínez Ocasio, kuiondoa Marekani katika ziara yake ya dunia kutokana na hofu yake kwa mashabiki kuvamiwa na wahamiaji.
Chanzo: Mwananchi Scoop